MAFUNZO KWA WANAHABARI
Tanzania Development and AIDS Prevention (TADEPA), kama shirika kinara katika kutekeleza mradi wa MTOTO KWANZA mkoani Kagera leo Machi 3, 2023 limetoa mafunzo kwa waandishi habari 5 mkoani Kagera ili kuweza kuandika kwa weledi habari za watoto wadogo.
Mradi wa MTOTO KWANZA unatekelezwa na TADEPA chini ya Shirika la Children in Crossfire Tanzania, kwa kushirikiana na Umoja wa Klabu za waandishi wa habari nchini (UTPC) na Shirika la Tanzania Early Childhood Development Network (TECDEN), ambao pia kwa pamoja wanatekeleza Programu hiyo jumuishi ya taifa.
Mkurugenzi wa TADEPA, Dr James Barongo Bashweka amewataka waandishi hao kuandika habari kwa usahihi na weledi, lakini akisisitiza juu ya kutafuta ufumbuzi wa masuala mtambuka yanayoathiri maendeleo ya mtoto.
Kwa pamoja washiriki wamekubaliana kuunda mpango mkakati kuhakikisha programu inawafikia wananchi kwa wingi, na wameunda kamati ya kulinda na kuboresha maudhui, na kufanya kazi kama timu, huku Mkurugenzi wa TADEPA akiahidi kuwasaidia waandishi hao kufika maeneo mbalimbali mkoani kwa ufuatiliaji na uchunguzi wa masuala ya watoto kadri mfuko utakavyoruhusu, na kuwa waandishi wengine wataongezwa kwenye timu.
Waandishi wa habari waliohudhuria mafunzo hayo ni Anord Deogratias (Kagera Community Radio FM), Theofilda Felician (Radio Karagwe FM), Anord Kailembo(Kwizera FM), Titus Mwombeki (Kasibante FM), na Mathias Byabato, Meneja wa Kagera Community Radio FM.